Na Brian Nzomo.

Joto la kisiasa lilianza kufumka pindi tume ya uchaguzi ilipotangaza kuwa shughuli za uchaguzi zingefanyika miezi tisa baadaye. Si barazani, si misikitini, si makanisani, si mikahawani, si mitaani. Kote kulitawaliwa na mijadala ya kisiasa.
Lakini mjadala uliozua zani kwa baadhi ya wakaazi wa eneo bunge la Mikalani ulikuwa kuhusu azma ya Bwana Shadrack Kishingo kugombea kiti cha ubunge kwa mara ya tatu. Bwana Kishingo alikuwa keshaketi bungeni kwa miaka kumi, jukumu lake kuwawakilisha wanamikalani. Licha ya umri wake mpevu wa miaka sitini, uchu wa uongozi wa tatu ulimlambatia ulimini.
Madaktari wake walikuwa wamemnasihi kutogombea tena lakini alitia masikio yake robota ya pamba. Hakupata kusikia onyo hizo.
Alisisitiza kuwa yeye alikuwa kijana barobaro, na kuwa mvi uliomkaa kichwani ulikuwa kwa sababu ya kula vyakula visivyo vya asili. Kila mkewe alipomsihi kutuliza azma yake ya uongozi mwingine, alijitetea kwa kusema,
“Mke wangu Selema, tazama jinsi nilivyo imara kama mbuyu. Unene wangu usije kudanganya kuwa sina damu yangu ya ujana.”
Makombora haya ya uzee wake yalimwudhi sana Bwana Kishingo. Akalazimika kuliacha mkongojo wake, na licha ya uchovu aliouhisi mgongoni na magotini, aliyavumilia ili watu wasimdhanie kabugia chumvi kupita kiasi.
Kila alipotazama kioo na kutazama kiakisi chake, alikereketwa kuona mvi zilizosheheni kichwa chake mithili ya unga mweupe. Alisalia kuilaani uzee, hakuficha chuki dhidhi ya uzee.
“Kwa kweli ujana ni moshi, waliamba wazee wa kale. Lakini kwanini? Kwa nini moshi hiyo inapita kwa kasi ya upepo? Ahhh…Ningejua siri ya kuwa kijana milele, singesita kufanya lolote ili hilo litimike,” alifikiri Bwana Kishingo.
Habari za mitaani zilizidi kumtamausha zilipofika masikioni pake. Sifa zake zilididimia na wengi walionekana kupoteza imani kwa uongozi wake. Wasaidizi wake wa kisiasa walipomweleza kuwa uchaguzi wa mwaka huo ungemwia vigumu kuushinda, alikasirika sana. Kwa hasira za mkizi, aliwapiga kalamu kwa madai ya kufanya kazi kisirisiri na wapinzani wake. Bwana Kishingo alikuwa ameamua. Hamna yeyote angemshurutisha kutogombea. Aliamini angeshinda. Asijue kuwa alikuwa sawia na chachandu aliyejipalia makaa moto. Na wakati ufikapo, angejichoma…
**** ***** *****
Magharibi. Wajihi wa jua ulianza kuchechea milimani. Wakulima na wavuvi walirejea nyumbani wamechoka tiki! Wameroa jasho lakini mioyoni mwao furaha ya kukamilisha kazi za siku hiyo bila dosari yoyote.
Lakini katika baa lake Bi. Masrufu kulichacha mjadala mzito baina ya wafuasi wa Bwana Kishingo na mpinzani wake Sam Kelebela. Sam alikuwa kijana barobaro. Mchangamfu na aliyechachawa azma ya kisiasa baada ya kusomea Chuo kikuu. Kule chuoni ndiko alikogombea na kushinda uongozi wa wanafunzi. Ikampa uzoefu na ari ya kugombea ubunge wa eneo la Mikalani.
“Huyo kijana hawezi kumwakilisha yeyote bungeni. Hata ubwabwa haujamtoka shingoni lakini anadhani amefuzu kutuwakilisha hasa sisi wazee? Haiwezekani!” alilaani Mzee Makupa akitema mate ardhini.
“Wewe Mzee usituletee ubozi hapa. Hivi hujui kuwa tupo katika karne ya Ishirini na moja. Karne ya teknolojia na mabadiliko ya Kidemokrasia. Na sharti tuwaondoe vizee vyote visivyojua lolote kuhusu uongozi wa karne hii,” alilalama Njengere akipiga fundo nzito la mvinyo.
“Uzee ni ishara ya hekima na busara. Mzee Shadrack ametuongoza vyema kwa mwongo huo alipokuwa mbunge. Mimi kura yangu nampa,”alisema Mzee Makupa kwa mashauo.
Vicheko vikawanda kwenye baa. Si vicheko vya furaha. La. Vicheko vya simango haswa.
“Eeh Mzee…watuvunja mbavu kwelikweli…ehh…,”alidakia Bi. Masrufu. “Hivi wewe kipofu nini? Tazama mandhari yako yalivyo. Ni lipi Mzee wako Kishingo alichokifanya kwa miaka yote hii. Hata bomba moja la maji hajapata kuwaletea. Wajukuu wako wangali teka maji mitoni kwa punda na mitungi.”
“Ahhh…Mzee umenimaliza. Ile barabara ya Katala aliyoahidi kuijenga katika mwanzo wa uongozi wake. Huu mwaka wa ngapi…” Njengere akaashiria kwa vidole, “Mwaka wa kumi vile haijapata hata kuona tingatinga ya ujenzi. Unataka kumpa miaka mingine mitano ya kutufilisi. Haya basi Mzee. Miaka mitano itapea. Wajukuuzo watazidi kuvuta pumzi ya vumbi kutoka barabara hiyo wanapoelekea shuleni.”
Kila mfuasi wa kijana Sam alitoa sababu za kumwondoa Bwana Kishingo. Lakini wafuasi wa Bwana Kishingo wakiongozwa na Mzee Makupa, walimgandama chaguo lao kama kunguni. Hawasikii tahakiki za wapinzani.
“Heri ibilisi umjuaye kuliko malaika usiyemfahamu usuli wake,” alighani kibusara. “Tuna imani naye Shadrack Kishingo.”
“Haya basi. Kumbuka kuwa sanda ya mbali haiziki mfu. Kwa miaka yote hiyo. Kishingo wenu ameyachuma matunda ya ufisadi wake. Mshahara mnono anaupokea ila hamjapata kumwona huku pindi uchaguzi ukamilikapo. Sasa kutatokea mabadiliko ya lazima. Mpende msipende. Sam Kelebela atakuwa mbunge wa eneo la Mikalani. Hata kama hili litatimika damu ikimwagika,” alifoka Njengere huku wafuasi wa Sam wakimpiga pambaja kwa lulu zake za kweli.
****** ****** *******
Kadri miezi ilivyopea ndivyo mchecheto wa kisiasa ulivyozidi. Kampuni zilinoga, kila mshindani akitamani ushindi. Bwana Kishingo alifanya bidii zaidi. Habari kuwa umaarufu wake ulikwisha pondeka hazikumfurahisha asilani. Lazima angeshinda. Kwa hila na hela. Nazo alizitumia barabara. Maajenti wake walipewa vitita vya pesa kuwahonga watu wamchague. Navyo vilimwagwa kama mtama kwa kuku wengi.
Si kina mama, si walevi, si vijana. Wote waliahidi kumchagua Bwana Kishingo. Bwana mkarimu kuwashinda wapinzani wake. Hamna kampeni iliyomgharimu zaidi kuliko ile ya Bwana Kishingo. Matrela ya utumbuizaji yalizunguka vijijini vyote eneo bunge la Mikalani. Wasanii waliotamba waliwaasa wapigakura kutowachagua maadui wa maendeleo waliompinga Mzee Kishingo. Nyimbo zao zilisheheni sifa tumbi nzima kwake Bwana Kishingo.
Kampeni za Sam Kelebela zilijawa semi za ahadi na ufanisi. Alitegemea ulimi wake ulioamba maneno mazito. Maneno yaliyojawa
maono. Hakujaribu kuwahonga. La. Hilo kwake lilikuwa kuzitemea mate sera za Kidemokrasia. Mikutano yake ilijaa vijana na kina mama walioona mwenge wa ufanisi kwake. Wengi wa waliomchukia ni walevi na wavivu waliopenda pesa za bure.
Bwana Kishingo hakutosheka. Licha ya kuwa meneja wa benki alimuonya dhidhi ya ubadhirifu wa mikopo aliyopokea pale, shinikizo la maajenti wake kufanya hima zaidi kwani Sam alikuwa akiendelea kupaa ilimpa wasiwasi zaidi. Hakuamini kuwa kijana mdogo, alikuwa akimpa hali mgumu. Juhudi zake za kujifanya barobaro hazikufua dafu. Ilhali zilimfanya aonekane amewehuka zaidi.
“Huyu mzee yupi anajifanya kijana ilhali joshi lake lilifuka kitambo? Eti kazungumza kwa mtindo wa kufoka,” wafuasi wa Sam walisimanga.
Hali hiyo ilimghadhabisha sana Bwana Kishingo. Lakini maajenti wake walimtilia shime zaidi. Hatimaye angeibuka mshindi.
Bwana mkarimu kuwashinda wapinzani wake. Hamna kampeni iliyomgharimu zaidi kuliko ile ya Bwana Kishingo. Matrela ya utumbuizaji yalizunguka vijijini vyote eneo bunge la Mikalani. Wasanii waliotamba waliwaasa wapigakura kutowachagua maadui wa maendeleo waliompinga Mzee Kishingo. Nyimbo zao zilisheheni sifa tumbi nzima kwake Bwana Kishingo.
***** ****** *****
Kipindi cha mwisho kiliwadia. Kampeni za mwishomwisho zilikuwa zikiendelea. Waingereza waliita abra hii the finishing power. Wengine wakaiita final touches. Kukawa kumezuka. Mara kwa Mara wafuasi wa mahasidi hao wa kisiasa walikutana kifahali. Wakizomeana na kupigana vikumbo na masumbwi.
Bwana Shadrack Kishingo alijawa wahaka zaidi. Yule mkurugenzi wa Kamati ya uchaguzi aliyekuwapo alihamishwa mara moja hadi eneo lingine. Hii ni baada ya Bwana Kishingo kumpa rushwa ya shilingi laki moja ili kuhakikisha ameushinda uchaguzi huo. Akaletwa mwingine. Huyu aliyeletwa alikataa kuhongwa. Abadan katan. Uchaguzi ungekuwa wenye haki na usawa. No irregularities, alitangaza kwa ujasiri. Kama ilivyokuwa ada kwa maajenti wake, walionenepa na kunenepeana kutokana na vitita vikubwa walivyofaidi, waliipakata nafsi yake. “Usijali Mzee wangu. Ushindi huu unao. Upo shantani mwako wallahi!”
Hatimaye siku ya uchaguzi ulifika. Kila mwanamikilani mpigakura alipiga foleni katika vituo vyote eneo bunge hilo. Kura mkononi. Kisha debeni. Kama alivyoahidi mkurugenzi wa Kamati ya uchaguzi, hakukuwa na ishara yoyote ya kadhongo kwa wapigakura. Maajenti waliwekwa mbali na wapigakura huku askari na makarani wa uchaguzi, Wenye macho ya mwewe, wamekaa ange kuzuia wenye raghba ya vurumai.
Shughuli ilipokamilika jioni, hesabu zikaanza. Sam Kelebela na wafuasi wake wametulia nyumbani kwake kijijini Mlopo kutazama matokeo. Shadrack Kishingo naye kijijini Bololo, ameshika tama kwa matarajio mbele ya runinga yake ya Sony. Amezingirwa na halaiki ndogo ya wafuasi na maajenti wake.
Alionywa na daktari. Ugonjwa wake wa shinikizo la damu utatarika zaidi iwepo angejihusisha na shughuli zitakazompa wahaka au furaha kupita kiasi. Lakini wapi! Maneno hayo yote yalikuwa kama kumpigia mbuzi zeze. Wataraji atacheza densi eti?
****** ******* ******
Saa sita usiku. Shughuli za uhesabu kura zilikamilika. Bwana Kishingo alighaya. Ametazama runinga huku machozi yakimlengalenga usoni. Moyoni, fundo nzito kama nanga lilisheheni. Ameshindwa. Haiwezekani.
Maajenti wake walimtazama kwa huruma na walijaribu kumchangamsha kwa kulalama jinsi uchaguzi huo ulivyofanyiwa hila na Sam Kelebela.
Punde si punde. Alihisi uchungu uliomkita kifuani na kumchechea pumzi. Aliyatoa macho yake pima. Akapiga ukemi wa uchungu. Waliokuwapo wakaanza kumnyanyua kutoka ardhini alimoanguka.
“Shadrack mume wangu usife. Help! Someone call an ambulance,” alipiga kite Bi. Kishingo.
“Selema mke wangu…,” alipumua Bwana Kishingo kwa nguvu. Pumzi zikimwishia Mzee wa watu. “Nimeshindwa…I’ve lost everything. Uchaguzi…Madeni…loans. Nitaishi vipi,”alilia Bwana Kishingo.
“Relax Shadrack. Usizungumze zaidi,” alilia Bi. Kishingo.
“Ondokeni Mzee apate hewa,” aliamuru ajenti mmoja aliyekuwa pandikizi la mtu, akiwasukuma umati uliolizingira gofu la Bwana Kishingo. Simba wa Mikalani yu taabani.
Kwa umbali, king’ora cha ambulensi kilisikika. Ving’ora hivyo vilitawaliwa na sauti za shamrashamra ya ushindi wa Sam Kelebela. Ngoma ziliwanda, nyimbo za ushindi zilighaniwa. Mbwembwe za kuusherehekea mwanzo wa miaka mitano waliyomkabidhi kijana wao. Simba wa kizazi Kipya amenguruma milimani…
******
Brian Nzomo ni mwandishi na mwanafunzi wa mawasiliano na uanahabari katika Chuo kikuu cha Kenyatta. Wasiliana naye kupitia anwani ya barua pepe: bryonzoms505@gmail.com