Na Brian Nzomo.
Machozi yakapukutika bila amri au tamanio langu. Sikutaka kuyafuta. Yatiririke tu!
Kuna mengi yamtafishayo binadamu. Huzuni, penzi lililotawanyika, usaliti, ugomvi, uchungu na kutowajibika ipasavyo. Ila, ipo hali imwekayo kabisa katika lindi la taabu kama njaa?
Njaa, si ya chochote kingine bali ile ya tumbo ihitajiayo chakula.
Nilipokuwa katika mwaka wangu wa pili katika chuo kikuu, ilikuwa si nadra kwangu kusalia njaa kwa siku zisizopungua mbili. Iwapo pia ningepata kula, chakula kingenimudu kwa saa chache tu!
Lakini jioni moja iliniweka katika hali ya kutamausha zaidi. Kwa siku mbili sikupata kukitia chochote tumboni ila maji tu. Mkoba wangu wa pesa ulikuwa mtupu. Hamna hata ndururu nobe ! Na kwa sababu zangu mwenyewe, sikupenda kuwaomba pesa rafiki zangu. Nilichukia deni !
Mchana kutwa nilishikilia imani kuwa mjomba wangu angenitumia angalau pesa kidogo za kunifaa kwa siku mbili. Aliniahidi kuwa alasiri au jioni angenitumia shilingi elfu mbili. Nilighairi njaa iliyonisokota na kupaa kwa anga za tumaini. Hatimaye ningepata kuizima njaa hii bila ya kumwomba yeyote usaidizi.
Nilipiga hesabu yangu kwa umakini. Shilingi elfu mbili. Hizo zilitosha kunifaidi hadi kikomo cha muhula ule pale chuoni. Huenda pia ningebahatika kupata kazi yoyote ili kuniondosha katika taabu hizi zisizokesha.
Alasiri ilifika. Simu mkononi ange kabisa, nikizisubiri pesa za mjomba wangu. Moyo unatumka huku nikiwaza na kuwazua. Je, iwapo hangepata kutuma pesa zenyewe, ningevumilia vipi kuingia siku ya tatu na njaa hii? Ningeamka kweli kitandani? Au ni nani angenisaidia?
Wakati huo niliwaogopa watu na hisani zao. Kila aazi ya binadamu niliichukulia kwa shauku kuu. Lakini siku hiyo, iwapo Ahadi za mjomba zingeambulia patupu, nisingekuwa na budi ila kuomba usaidizi kwa wale niliowafahamu kuwa rafiki zangu.
Anga ikabadilika jioni ilipoanza kuingia. Weusi wa kaniki ukatwaa na kuwanda kote. Niliketi kwenye upembe mbali kidogo na lango la chuo nikiwatazama wanafunzi wengi wakiingia na kutoka, nyuso zao zikiashiria uchangamfu na bashasha. Niliwahusudu sana. Nikawaza ni lipi liwatengalo wanadamu? Kila mja ana taabu zake mwenyewe! Lakini taabu za wengine hazikuwagubika na kuwamega kutishia kuwaangamiza! Ila taabu za wengine ziliwaauni wengine kama zimwi lisiloazimia kukusaza.
Nikasubiri kwa muda mrefu. Saa moja jioni ikaingia. Hamna pesa zozote zilizotumwa. Nitafanya nini miye mja mlitima? Niliwaza nikimeza mate machungu.
Nilijizoa pale upembeni nimeghafilika si kidogo. Nikatembea aste kwa shida kuelekea kwenye beni. Huenda niliyeishi naye pale angenifaa siku hiyo. Jioni moja hii ! Mbele sikuona vyema. Macho yangu yalikuwa kana kwamba yametiwa moshi. Machozi yakapukutika bila amri au tamanio langu. Sikutaka kuyafuta. Yatiririke tu!
*********
Kwa bahati nzuri au mbaya, nilimkuta mwenzangu Tony akijitayarisha kuondoka chumbani. Amevalia fulana kuu nyeusi na chepeo lililokuwa na maandishi Golden state warriors. Sikumwomba usaidizi ghafla kwani jambo hilo lilikuwa adimu kwangu kufanya.
“Waondoka eti?” niliuliza kiutani.
“Naam,” alijinibu. “Kuna rafiki yangu tuliyesoma naye chuo cha upili ameandaa sherehe ya kukata na shoka pale Kahawa Wendani!”
Sherehe. Chakula. Mlo. Nilitabasamu.
“Tony,” nilianza kwa utaratibu. “Ningependa kukuomba angalau unifae kwa shilingi hamsini, au thelathini tu nipate kula chajio, tafadhali!”
Tony alinitazama kwa dharau sijui kwa sababu ipi. Tangu mwanzo wa muhula huu nilipoanza kukaa naye pale benini, hakukuwepo ishara ya mkwaruzano baina yetu. Si eti tulikuwa na mazungumzo mengi pia, lakini sikupata kumtendea ubaya wowote.
“Sikiliza mwenzangu,” alinisuta. “Wewe ni mtu mzima. Una wazazi wako, nina wazazi wangu. Kwa nini unanikopa pesa miye? Hulishwi au vipi?”
Maneno yale yalinichoma moyo. Kwa utepe fulani, yalisheheni ukweli. Kwa nini? Kwa nini wazazi wake Tony walimudu masomo yake na kumpa pesa za kutosha kupata shibe pale shuleni? Ila miye, niliyekuwa na wazazi wote wawili, nililalama njaa? Lakini ningefanya nini? Nilipomweleza baba matatizo yangu, alinieleza pia matatizo yake yaliyofaa kusuluhishwa kwa pesa zisizopatikana kama siafu kiangazini.
Kwa vile sikuzoea kumwomba yeyote usaidizi, sikung’ang’ana sana kumshawishi. Ingekuwa jambo la soni sana kumwomba usaidizi mtu asiyenuia hata kufanya hivyo. Nilinyamaza kimya na kuwawaza waja wengine.
Tony alipoondoka, niliachwa nimesononeka kiasi cha kwamba sikuamini kuwa ningepata usaidizi.
‘Nimpigie nani simu?’ nilifikiri kwa mapana. Lakini kila jaribio lilionekana kunishusha tumaini.
Nilipiga simu tatu. Kwake Leon, ambaye alinieleza kwa upole kuwa hangepata nafasi ya kunisaidia kwani alikwisha safiri kijijini. Nikamjaribu Willy, lakini simu yake hakushika. Mwishowe nikamtafuta Victor. Akanieleza kuwa bado yu benini kwake anakusudia kuenda kupata chajio sokoni. Akanieleza nimsubiri kwenye lango la kutoka chuoni ili nimsindikize kule. Nikashusha pumzi na kuvaa jaketi langu kwa pupa.
‘Victor ni somo wangu,’ niliwaza. ‘Atanisaidia kwani tulisoma naye chuo cha upili na nilimsaidia kwa namna yoyote wakati ule. Ni abra yangu kutendewa wema’
Kibaridi kilinichuna niliposubiri langoni. Ilikuwa saa mbili usiku. Sikujua iwapo kibaridi kilitokana na hali ya unyevunyevu uliokuwepo, au ni uhafifu ulioniwamba kutokana na njaa. Nilijiahidi kunyenyekea.
Willy alipofika pale, nilitaka kumweleza masaibu yangu kabla ya kuambua nyayo kuelekea sokoni lakini hakunipa nafasi ya kuzungumza. Alitaka azungumze yeye. Akanipa visa vyake vya kipuuzi. Jinsi alivyomsasambua mhadhiri wa kike, jinsi alivyomlazimisha msichana mwenye uja uzito wake kuuavya. Havitoshi vitimbi vyake. Lakini nilizisikiliza kwani mwenye njaa hana budi ila kupashwa vioja. Hana chaguo !
**********
Mikahawa mingi ilikuwa imefungwa ilipofika saa tatu usiku. Michache tu ndio iliyokuwa imefunguliwa. Na hii ilikuwa ile iliyouza vyakula vyao kwa bei ghali. Lakini Willy hakujali kuhusu hilo. Nikaingia naye katika mkahawa uitwao Pinewood restaurant.
Mkahawa huu ulikuwa na meza zilizoundwa kwa mbao laini na kurembwa kwa aina fulani ya feruzi. Hewa yake ilihanikiza harufu nzuri ya vyakula vilivyopikwa kwa umahiri mno. Orodha ya vyakula ilionyesha kuwa mkahawa wenyewe ulipania kuwahudumia wateja wenye hela zaidi.
‘Mmh ! Pilau, nyama ya kubanika na sharubati. Waonaje?’ alinisaili.
‘Sioni tatizo navyo iwapo una fedha tosha za kuvigharamia,’ nilijibu kwa kutabasamu.
Willy akamwiita yule mhudumu na kuagiza chakula chake tu! Sikulalama wala kumaka. Mja hazijui shida za mwengine hadi atakapoelezwa. Willy hakujua tatizo langu. Nikaamua ni fursa mwafaka kumdokeza.
“Mwenzangu, nina shida na ningependelea unisaidie, najua si kawaida yangu kuomba usaidizi kwa yeyote yule lakini…” nilianza kueleza.
“Ndio sababu iliyofanya nikuite hapa nami,” alinikatiza akicheka.
Nikashangaa. Huenda alijua kuwa nina njaa kuu iliyohitaji kuzimwa! Tumaini likapea.
“Sikiliza rafiki yangu,” alisema. “Naelewa hali ya mwanafunzi hapa chuoni si ya kupendeza mno. Kila mmoja wetu ana shida nyingi, ila ni sharti tuzame katika anasa kama tutakavyofanya hivi leo! Ni Ijumaa eti!”
“Si hivyo mwenzangu!”
“Aa-ah! Sikiliza bro. Nikimaliza kula chajio, twaelekea moja kwa moja hadi Dimples. Hebu sikiliza kwa umbali jinsi hepi ilivyonoga katika kilabu hiyo. Hebu sikiliza…”
Nikashusha pumzi. Kwa umbali, ngoma zilichacha takriban mita hamsini kutoka pale mkahawani. Kilabu ya Dimples ilikuwa bahari ya wanafunzi kila Ijumaa, au hata Jumamosi. Nimeingia kilabuni mle mara kadhaa lakini nilikawia kuenda kule kutokana na shughuli mzo za kimasomo na uchechefu wa pesa.
“Nina njaa bro!” niliamua kuvunja utoelewano uliokuwa baina yetu.
Willy alipokea mlo wake akitabasamu. Akapiga funda la kwanza ya sharubati yake.
“Aaah! Utamu wa pesa! Vyakula vitamu, mivinyo yenye hadhi na wanawake kwa wingi! Wasemaje tena mwenzangu! Eti una njaa?”
Nilitikisa kichwa changu kuashiria ‘ndio’. Mdomo wangu ulianza kupapa kutokana na uhafifu.
“Mimi pia, nina njaa. Sijapata kujilaza na mwanamke kwa juma nzima!”
“Si njaa ya aina hiyo,’ nilianza kuhisi ghadhabu ikitamba katika sauti yangu.
“Haya basi!”
“Njaa ya chakula. Sijakula chochote kwa siku mbili yaelekea tatu! Nisaidie angalau shilingi mia, au hata hamsini nipate kukitia chakula tumboni !’ nilisema huku nikizuia kilio kuniafiki.
Willy alinitazama kana kwamba haniamini. Akawa kimya akaendelea kula chakula chake kwa utaratibu. Njaa yangu ikazidi maradufu. Kichwa change kikawanga. Kikaenda darmadaru. Tumaini langu likavunjwa upya. Nikanywea.
Alipomaliza kula, alijizoa pale alipoketi na kusimama. ‘Hebu twende Dimples uache maneno mengi. Sitaki binti wazuri watekwe wote wasalie vishata!’
Sikuamini masikio yangu. ‘Lazima hii ni ndoto mbaya,’nikatanabahi. Rafiki. Rafiki. La! Sina rafiki hapa!
“Hata mia mwenzangu huwezi nikopesha, lakini u radhi kununua pombe?” nikasema kwa uchungu.
“Waenda Dimples, huendi?” akaepuka swala tena.
Sikusema zaidi. Nilielekea mlango wa kushoto wa mkahawa na kutokomea gizani. Nikaazimia kurudi benini. Ninywe maji nilale. Lakini usingizi upi utakuja ? Tumbo tupu !Siwezi tena, nikajisemea. Iwapo singeamka asubuhi siku itakayofuata, ingekuwa jambo la heri sana.
*********
Maji yalinijaa tumboni. Pomoni.
Nikaazimia kulala. Tony hakuwa amerejea bado. Ila halikuwa jambo la kunipa wahaka. Nikalewa kwa kiasi fulani cha inda. Nikaichukia ulimwengu na walimwengu. Kwa nini mwenye haja ana upweke namna hii !
Nilipokuwa nikiivuta blanketi yangu, kichuma fulani kama sarafu kilianguka sakafuni ting !
Nikainama bila kuambiwa na kukitafuta. Nikakizoa kutoka mvunguni.
“Shilingi Kumi!” nilifurahi na kujisemea.
Nilipokitazama kichuma kile mwangazani, nilimeza mate machungu.
Ilikuwa shilingi moja. Haiwezi nunua hata peremende katika janibu hizi.
Kitandani, machozi tu! Mawazo! Kifo!
Nikatamani Izraili anichukue usiku huo. Lakini, kama rafiki wasiotegemeka katika hali za dhiki, akaniepuka tena nikaamka asubuhi. Sina nguvu. Nidhamu yangu hata hivyo ikachujuka. Nilijizoa kitandani ghafla. Tony hakuwa amerejea.
Nikainama mvunguni na kulivuta shanta lake. Nikaanza kutafuta sarafu zozote ningepata pale. Mlango ukafunguliwa. Tony akanikabili nikiikamata mkononi shilingi elfu moja yake. Tukatazamana. Njaa ikapambwa na soni na woga.

Good article brother with lots of realiy
LikeLiked by 1 person