Na Brian Nzomo.

Ni dhahiri kuwa nchi yetu ilikuwa imefikia upeo wa vurugu na ghasia. Kila pembe ya nchi hii ilikuwa inarindima kwa nyimbo za uasi.
Waondoke, wang’atuliwe,
Tuwasake, tuwaondowe,
Wabinafsi na mabepari
Wasipate tena kustawi
Wala kunawiri,
Wasio na tofauti na wachawi…
Nchi iliyojulikana kwa utulivu wake katika bara zima tangu enzi za jadi. Nchi hiyo sasa imefurika damu ya viongozi na wananchi wao. Taswira za kutisha zilionyeshwa kwa runinga za ndani na nje. Jiji la Manaki liligubikwa na mifyatuko ya risasi, vilio vya simanzi na uharibifu usioeleweka.
Majuma matatu yamekwisha tangu hali hii ya sintofahamu kuanza. Japo haikuwa jambo la kushangaza kwani ishara zote zilidhihirisha kuwa wananchi walikwisha choshwa na uchumi uliodorora huku viongozi wakijihusisha na ubadhirifu wa mali ya umma.
Lakini wimbi hili lilianza vipi? Limepata nguvu haraka licha ya juhudi kali za serikali kulizima. Wiki tatu zilizopita, ndipo tembe alipotetea. Hali tete ikaanza.
******* ******* ****
Ishara hazikuanza kudhihirika kwa mpigo bali hewa ya ghasia ilianza kuhisiwa kwa muda mrefu. Malalamiko na minung’uniko ilisikika kote, midomo ya wananchi ikirindima kwa ghadhabu. Nchi hii inakwenda wapi? Waliuliza. Jinsi siku zilivyopea ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya zaidi. Umasikini ukazidi kuwamega wengi na kuwasakama zaidi. Mifuko ilichechea hela na njaa kuwasokota zaidi. Uchumi ukaporomoka zaidi na kampuni nyingi kulazimika kufungwa. Ukosefu wa kazi ukawa maradufu. Visa vya kujitoa uhai vikafumka. Wananchi wakaililia serikali. “Tusaidieni!” Lakini wapi! Serikali ilikuwa na shughuli muhimu za kutekeleza. Ilikuwa na miradi kabambe iliyofaa kupewa kipaumbele wala si kusikiliza vilio vya wananchi wavivu.
Miradi ya barabara na reli ilihitaji hela nyingi zaidi. Madeni yakakopwa kwa nchi za kigeni. Iwapo hazingetosheleza azma ya serikali, ushuru ukaongezwa kwa bidhaa muhimu. Bidhaa hizi zikawa ghali kwa kiasi ambacho wananchi hawangeweza kumudu. Hasira zikawa si chache.
Hatimaye rais akahojiwa na vyombo vya habari. “Ana mipango ipi kuiokoa nchi iliyozama kwa beluwa iliyofurika?” Rais akacheka. Kisha kwa mashauo akasema, “Sielewi ni kwa nini wananchi wanalalama. Njaa ipi? Mkate ni shilingi Mia tano tu…” Jibu hilo liliwatamausha wengi. Mia tano tu? Walimaka. “Mkate wenyewe ni shilingi sabini Sasa hivi. Hii ni baada ya kufumka kutoka shilingi arubaini…”
Haijulikani vijikaratasi vya uchochezi vilitokea wapi, Lakini uchochezi ulipashwa kote. Mikutano ya watu ilikutana nyakati za usiku na kuandaa azma ya mageuzi. Imetosha. Imetosha. Yafike kikomo . Ghasia zikaanza. Huenda serikali ilidhania kuwa ni vurugu ya kawaida ambayo ingezimwa kwa siku mbili tu. Walikosea. Majuma matatu yameifanya serikali ikatetemeka. Walijaribu kuzungumza na kiongozi wa chama cha mageuzi. Kijana barobaro Gallant Mutesi. Lakini akakataa. “Hamna mazungumzo. Muondoke Mara moja…” Rais akaghadhabishwa. Akaamuru jeshi ilizime wimbi hili. Lakini nguvu na azma ya raia ikawanuia vigumu. Baadhi ya viongozi wa Kijeshi wakahofia kuwa mageuzi yangetendeka kwa lazima. Wakawa hawana budi ila kuwaunga wanamapinduzi mikono…
****** ****** ******
Rais Munyi Kabase alikuwa ofisini mwake akiwatazama mawaziri wake wawili walioketi kwa wahaka, kila mmoja ameyatunda macho yake ukutani. Walikuwa kimya. Waziri wa uchumi na biashara na waziri wa Usalama.
“Hebu niambieni ni kwa nini niliwaamini kuihudumia serikali yangu, iwepo mmeshindwa kurejesha hali kama ilivyokuwa? Niambieni!” Rais alisema kwa hasira. Mawaziri wakasalia kimya. Kila mmoja hana la kuamba.
“Tazameni magazeti. Tazameni! Tazama jinsi vyombo vya habari za kilimwengu vilivyotangaza ghasia hizi. Tazama! Tazama jinsi serikali yangu ilivyotapakazwa tope na wanahabari na watetezi wa haki…” Rais akawatazama kwa tabasamu ya kejeli. “Haya yote yanafanyika kwa sababu mnazembea! Na yu wapi waziri wa mawasiliano? “
“Amejiuzulu mheshimiwa rais,” alidakia waziri wa uchumi.
“Kujiuzulu? Na yu wapi wa masuala ya Kigeni?”
“Kajiuzulu pia mheshimiwa rais,” akadakia waziri wa Usalama.
Rais akawa kimya kidogo. Akashusha pumzi na kujisemea mwenyewe, “Hata Mlange? Yule nilivyomdhania binamu wangu wa kweli ameniacha niungue kwa moto hii?”
Akafikiria kidogo. Hakuamini kuwa mwenge wake ulikuwa karibu kuzimwa na raia. Hakuamini kuwa wananchi waliojisabilia mwake kwa miongo mitatu ya uongozi walikuwa tayari kumng’atua enzini. Alishangaa ni kidudu gani aliyekuwa na ushawishi mkubwa namna hii kwa kiasi cha kuwachochea raia kufanya mapinduzi. Raia waliyomtii vikali . Na licha ya nyingi inda na inadi alizowatendea, hawakupata kumwiinukia hata Mara moja. Au huenda ni wazungu? Lazima. Wale waganga weupe waliowaloga waafrika na sirihi za Kidemokrasia. Alishangaa. Wazungu walivyomsifia mara kwa mara kwa mahusiano mema aliyofanya nao. Kweli wale watu wajanja kweli. Wana hulka za lumbwi.
“Bwana Rais,” alimzindua mawazoni waziri wa Usalama, “Nasi pia twashukuru kwa hidaya uliyotutunukia kwa kutuajiri…Kwa taadhima kocho twakushukuru…Lakini nasi pia tunajiuzulu Kwani hali si hali. Wananchi wengi wameuawa tayari. Na kulivyo sasa hivi, hakuna ishara yoyote ya kuwa serikali yako itadumu. Kuta zimeporomoka tayari. Hizi hapa nyaraka za kujiuzulu. Tunakusihi pia…Iwepo unaipenda maisha yako, jiuzulu pia.” Mawaziri hao walisimama na kuondoka mle ofisini. Rais aliachwa ameachama. Serikali yake ishakuwa gofu. Tumaini limefifia zaidi.
Akahisi uchungu moyoni. Miongo mitatu. Mali ya umma amezoa kwa wingi. Viganja vyake vimejaa damu ya wengi. Akilini mkarindima wimbo aliousikia kwa runinga. Wanamapinduzi waliimba kwa hasira.
Waondoke, wang’atuliwe,
Tuwasake, tuwaondowe,
Wabinafsi na mabepari
Wasipate tena kustawi
Wala kunawiri,
Wasio na tofauti na wachawi…
Akahisi fundo moyoni. Akauma mdomo wake wa chini kwa hasira na kupiga ukelele. “Waangamizwe wasosholisti na wakomunisti. Mashetani hao. Maradhi ya taifa”
Punde si punde, mlango ukafunguliwa na wanajeshi watatu waliojihami vilivyo wakaingia. Yule mrefu aliyeoonekana kuwa mkuu wao akaamuru kwa sauti nzito kama radi.
“Mheshimiwa rais Munyi Kabase. Unahitajika sebuleni sasa hivi…” Akajua yamemfika yaliyowafika wengi kama yeye. Mapinduzi yamekamilika.
Taifa lilipotangaziwa habari kuwa Rais Kabase ameachia madaraka, hali ya furaha na buraha ikarejea. Wamewapoteza wengi. Waume kwa wanawake. Watoto kwa wazee. Lakini damu zao hazijafurika bure. Dikteta ameondolewa.
Yu wapi wananchi wenzangu wapendwa,
Yule dikteta katili na mbinafsi kaondolewa,
Mama yangu eh, baba yangu eh,
Tudensi kwa mikogo Kwani tu huru eh…
Akafikiria kidogo. Hakuamini kuwa mwenge wake ulikuwa karibu kuzimwa na raia. Hakuamini kuwa wananchi waliojisabilia mwake kwa miongo mitatu ya uongozi walikuwa tayari kumng’atua enzini. Alishangaa ni kidudu gani aliyekuwa na ushawishi mkubwa namna hii kwa kiasi cha kuwachochea raia kufanya mapinduzi.
**** ****** ****
Serikali ya muungano iliundwa ili kuipa tume ya uchaguzi muda wa kufanikisha uchaguzi wa kiraia. Kiongozi wa raia Gallant Mutesi pamoja na wa kijeshi Jenerali Mathias Ndara wakawachagua mawaziri changamano. Vyombo vya habari za kilimwengu vikadokeza kwa furaha kuwa wanawake kumi walichaguliwa kama mawaziri. Taifa letu likawa ishara ya Uhuru na demokrasia Afrika.
Serikali mpya haikupoteza wakati kuwaandama vikaragosi wote wa utawala uliobwagwa. Wengi wakapokwa mali zao ikiwemo rais Kabase. Wengine wakafunguliwa mashtaka ya ufisadi na udhalimu wa kiuchumi. Shoka ikawatema wote bila huruma. Raia nao wakachachawaa kila habari ilipotangazwa kuwa haki ilitendeka.
Mambo yakarejea vyema tena na macho ya ughaibuni yakaondolewa kwetu. Ila haikutangazwa mizozano kati ya viongozi wa Kiraia na kijeshi. “Wale ni watu wenye busara. Watatatua migogoro iliyopo…” raia walijipa tumaini. Hadi pale mwezi mmoja ulipokwisha…
Alfajiri. Saa kumi na moja nilikuwa nafungua duka langu tayari kuianza shughuli ya kujenga taifa. Redio yangu ya Sanyo ilikuwa ikinitumbuiza kwa nyimbo za kusisimua. Mtangazaji akadakia na kutangaza habari zinazochipuka.
“Asubuhi hii mpenzi msikilizaji habari zimefika katika chumba chetu cha habari kuwa jeshi imewakamata wakuu wote wa raia na kuwafungia kusikojulikana kutokana na madai ya kujaribu kuyasaliti mapinduzi. Mkuu wa jeshi Jenerali Mathias Ndara ametangaza kuwa serikali imechukuliwa rasmi na jeshi na kuwa raia wameombwa kutulia hadi pale hali itarekebishwa…Mengi zaidi tutakuarifu pindi tuipatapo habari hii kwa kina. Jina langu ni Denis Mondi…”
Mapinduzi haswa! Dikteta hadi mwingine. Demokrasia nchini kwetu itasalia hadithi za watoto.
Brian Nzomo ni mwandishi na mwanafunzi wa mawasiliano na uanahabari katika Chuo kikuu cha Kenyatta. Wasiliana naye kupitia anwani ya barua pepe: bryonzoms505@gmail.com.