Na Brian Nzomo.

|Bright news.
“Situmahi kukuona hapa hivi karibuni. Miaka kumi na mitano ni mingi sana. Hata hivyo kuna tumaini. Tumaini ya kuwa utarekebisha mkondo wa maisha yako na kuwa mwananchi mwema na mwadilifu…” alidokeza yule afisa wa magereza akimkabidhi Simiyu shanta lililosheheni nguo zake. Suruali moja mararumararu na shati la buluu lililochanika. Hizo ndizo mali alizomiliki katika dunia hii. Dunia alimoishi kwa miaka thelathini na tatu.
Alipotembea kuelekea kwenye lango la gereza, aliwaona wafungwa wengine wakimtazama kwa macho ya gere. “Ana bahati huyu…” walinong’ona. Wengi wao aliwapata pale miaka kumi na mitano iliyopita. Wengine waliletwa majuzi. Mahabusu hawa wa gereza kuu la Shivatsa, aliojumuika nao na kuvumilia nao katika hali duni iliyokuwa ibada katika magereza ya taifa hili. Katika gereza hili, aliunda urafiki na pia mahasidi na wengine. Alijifunza useremala na vilevile uhalifu wa mbinu za kijanja. Hatimaye, muda uliwadia wa kifungo chake kukamilika. Anarejea nyumbani sasa. Kwa boma la mzee wake Titus Shikhanda. Atapokelewa vipi? Alijiuliza. Watamkumbuka kweli yule kijana barobaro wa miaka kumi na nane, aliyewatia soni kwa kujihusisha na uhalifu na kulazimika kula kalenda?
Alipoondoka langoni mwa gereza, alivuta hewa kwa nguvu na kuishusha pumzi kwa nguvu. Hatimaye, hewa ya Uhuru. Alihisi miguu yake ikisisimka kwa furaha ya kupata kutembea juu ya ardhi huru. Lakini moyoni alihisi hofu iliyomkita tangu jioni iliyopita. Maisha yake yangeanza upya kwa namna gani? Familia yake itampa motisha na nafasi ya kujipa maisha? Au watamtema kama mwana mpotevu asiyekubalika? Alijua vyema hasira za babake. Yule mzee hakupenda mzaha na aibu asilani. Angemsamehe kweli?
Alitembea kwa hatua ya polepole kuelekea stanini. Hapo angeabiri basi la kuelekea Amagoro. Kisha angeabiri bodaboda ya kuelekea kijijini kwao Shivale. Simiyu alizongwa na mawazo mazito ya jinsi hatma yake ilivyomwafiki. Miaka kumi na mitano iliyopita…
****** ******* ******
David Simiyu alikuwa mwana wa tatu wa mke wa kwanza wake Mzee Titus Shikhanda wa Shivale. Enzi hizo, Mzee Shikhanda alikuwa mkulima tajika wa miwa na mzee aliyeheshimiwa sana katika kijiji hicho. Licha ya kuwa na mali ya kutosha kuilisha familia yake kuu, Mzee huyu hakulegeza azma ya kuwatia shime wanaye kusoma kwa bidii. Alikuwa mzee mwenye maono kwani pia bintize walipata kuona milango ya shule; msingi hadi kile kikuu. Nao walifanya bidii wasije wakamwaibisha baba yao.
Mwanzoni Simiyu alikuwa wembe masomoni. Alikuwa hajasenea hata kidogo katika elimu. Alipoingia shule ya upili ya Makhandia, iliyokuwa na sifa tumbi za uhodari, ndipo anga yake ya masomo ilianza kupata giza na nyota yake kufifia. Mzee wake wakati huo alikuwa hashughuliki sana na masomo ya wanaye kwani sekta ya sukari ilianza kuingiwa beluwa. Nyakati nyingi alisafiri hadi mjini Nairobi kukutana na viongozi na maafisa wa wizara ya kilimo. Hivyo basi, kudidimia kielimu kwake Simiyu kulimpita mzee Shikhanda. Jinsi alivyozidi kusonga kwa hatua za shuleni, ndivyo elimu ilivyozidi kumwiia vigumu Simiyu.
Alipofika kidato cha nne, Simiyu alikata ushauri kuwa masomo si hidaya yake. Akaanza kushirikiana na wanafunzi watoro kusababisha hali tete shuleni. Si kuwapiga wanafunzi wengine, si kuwatishia wafanyikazi, si wizi, si utumizi wa mihadarati, si utotiifu. Vyote walivifanya. Alifukuzwa shuleni kwa muda mara mbili. Kila mara alibahatika kumkosa mzee wake nyumbani kwani huo ndio ungekuwa mwisho wa kupotoka kwake.
Lakini upeo wa uhalifu wao ulifika mwaka huo mwezi wa Septemba. Simiyu pamoja na watoro wenzake waliandaa mgomo hatari usiku na kuwapiga walimu vibaya. Katika hali hiyo, nyumba kadhaa za walimu zilitiwa moto na mwalimu mkuu Bwana Sylvester Wanjala akateketezwa ndani ya gari lake. Polisi na wanahabari walipofika walipigwa na mughma kuona uovu uliotendeka. Uchunguzi ulipofanywa, Simiyu na rafikize walikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kusababisha ghasia na mauaji ya mwalimu mkuu Bwana Wanjala. Walikiri kortini kuwa walifanya hivyo na walifungwa kila mmoja miaka kumi na mitano.
Simiyu alikumbuka uso wa wazaziye na umbu zake pale kortini. Zilijawa tahayuri. Mwanao kageuka afriti. Nduguze wakuu walikuwa wamefanikiwa maishani na walikuwa wana kazi zenye nafasi na hela nzuri. Lakini yeye, yeye alikuwa mahabusu aliyeachiliwa. Asiye na maisha. Naye arejea nyumbani. Hajui kitakachomfika kule.
“Mzee, unaenda Amagoro au Khalilindi?” Aligutushwa kutoka lindi la mawazo. Akashangaa na kutamaushwa kuitwa mzee. Kwani kulimkumbusha kuwa ujana wake umefikia upeo ilhali hakuwa na chochote cha kujivunia. Aliabiri gari bila jibu na kuanza safari yake.
Simiyu alikumbuka uso wa wazaziye na umbu zake pale kortini. Zilijawa tahayuri. Mwanao kageuka afriti. Nduguze wakuu walikuwa wamefanikiwa maishani na walikuwa wana kazi zenye nafasi na hela nzuri. Lakini yeye, yeye alikuwa mahabusu aliyeachiliwa. Asiye na maisha. Naye arejea nyumbani. Hajui kitakachomfika kule.
******* ******* ******
Simiyu alifululiza moja kwa moja hadi kituo cha bodaboda mjini Amagoro. Ilikuwa adhuhuri na licha ya njaa kali iliyomsokota tumbo na kumwanga kichwa, hakuwa na pesa za kutosha kuingia mkahawani kupata chamcha.
Waendesha bodaboda alikuwa wakipiga soga za kisiasa wakibishana vikali kuhusu wanasiasa waliowaunga mkono. Simiyu hakujua ni vipi rafikiye wa zamani Johana Matendechero alivyomfahamu lakini alisikia amemwita jina lake kamili. Waliamkuana kwa furaha huku Matendechero akiwa tayari kumpeleka kijijini.
Walizungumza kwa kirefu kuhusu mengi yaliyotendeka kwa miaka hiyo yote Simiyu alikosekana kijijini. Matendechero alimweleza Simiyu kuwa babake na mamake mzazi walifariki miaka kadhaa iliyopita. Simiyu alisikitika sana kwani walifariki kabla ya kuwaomba msamaha kwa kupotoka kwake. Kijiji pia kilibadilika sana baada ya Richard Khavala nduguye mkuu kunyakua ubunge wa eneo hilo. Barabara zilijengwa, umeme ukaletwa na kila boma likapata mabomba ya maji. “Maendeleo tosha,”alisema Matendechero.
Kwa muda kidogo, Simiyu akawa kimya. Aliwaza kwa kina. Huenda nduguye angemsaidia. Akamwaagiza Matendechero ampeleke kwake. Matendechero akafanya hivyo. Alijua kuwa Richard alikuwa nyumbani kwani vikao vya bunge vilisitishwa kwa muda wa likizo.
Walipokuwa njiani, Matendechero alimwaamkua mvulana mmoja mwenye wajihi wa kuvutia na aliyejawa siha. Kisha akamuuliza Simiyu,
“Wajua yule kijana?”
“La!” Simiyu alijibu.
“Yule ni mwanaye Cecilia…”
“Cecilia?” Simiyu aliwaza kwa muda. Cecilia aliyemjua vyema ni msichana mmoja mlimbwende aliyemwenzi sana katika shule ya upili. Hakujua iwepo Cecilia alimwenzi pia lakini hakujali hilo. Alilemazwa nafsi na sihiri za binti yule akakosa tiba. Mara ya mwisho kuhusiana naye ilikuwa mwezi mmoja kabla ya mgomo ule. Ilikuwa likizo ya Agosti anayoikumbuka vyema. Saa kumi na mbili thenashara jioni, wawili wao walikuwa mle katika shamba la miwa. Wakila uroda wa ujana wao.
“Yule kijana ana miaka kumi na minne. Inasemekana Cecilia alipata uja uzito wakati huo kabla ya kufungwa kwako. Licha ya kuwa alisema Bwana Handas Shikhulia ndiye baba wa mtoto, wengi hawakuamini. Sura hii ilikuwa inashahibiana na yako wewe…” Matendechero alisema akichekacheka. Simiyu hakutaka kuzungumza zaidi kuhusu hilo.
“Cecilia ni muuguzi katika hospitali ya Kakamega….” Simiyu alighuna tu. Alitaka kuonyesha kutopendezwa na mazungumzo kumhusu Cecilia. Matendechero alikuwa nusura ampige dafrao mbuzi aliyememera ovyo ovyo katikati ya barabara. Matendechero alikasirika na kusema kwa hasira,
“Hawa watu fuchinga wanaachaaacha mbuzi zao kwa parapara ndio zikikonkwa wanaenda kwa chief kuitisha malipo…Fchinga sana…”
******* ****** *******
Simiyu aligundua kuwa nduguye hakufurahi kumwona. Licha ya kuwa alijaribu kuficha chuki iliyomsinga moyoni kwa kuchekacheka naye, matendo haya yote yalionekana wazi kulazimishwa. Matendechero alibugia sima kwa nyama kwa ulafi wa fisi huku akimsimulia mbunge wake matatizo yaliyomkumba. “Pwana mheshimiwa. Iko mitoto yangu iko kwa nyumba kwa sababu imeshindwa kupata pesa ya uniform…Mimi naompa tu usaidisi kitoko. Na mungu atabariki wewe…” Richard alitabasamu tu na kuahidi kumpa shilingi elfu tano. Matendechero alifurahi zaidi ya kufurahi na akaondoka kuendelea na kazi. Simiyu na nduguye Richard wakasalia pekee yao. Simiyu akaichukua kama abra ya kuzungumza mambo ya kifamilia. Akamweleza kuwa amerejea kutafuta maisha mapya kijijini na kuwa angependa angalau usaidizi mdogo wa mtaji na kikonde aanze maisha. Alisema pia alikuwa mahiri katika useremala na mtaji wa kujengea karakana pia ungemfaa pakubwa.
Richard akasimama. Akaelekea upande mwingine wa sebulena kutazama picha la babake lililotundikwa ukutani. Mzee Shikhanda. Mzee wa wazee kijijini Shivale. Akamtazama Simiyu na kusema kwa upole, lakini kwa uchungu.
“Wajua kuwa baada ya wewe kupelekwa gerezani, maisha ya baba hayakuwa kama awali. Alianza kunywa mvinyo kwa wingi ili kupunguza uchungu aliouhisi moyoni juu yako. Mama naye akanyanyapaaiwa na kina mama wenzake kwa kuwa mwanaye ambayo ni wewe, alikuwa muuaji,”
Simiyu alitazama chini kwa haya. Akaghuna, “Nimetubu kila kosa nililofanya na ninahisi mtulivu kwani nimewajibikia yote niliyofanya kwa kifungo changu, naomba unisamehe ndugu yangu…”
Richard akamtazama kwa jicho la hasama. Akasema kwa ghadhabu, “Umekuja huku kufanya kitu gani? Niambie! Huna polite huku. Uliyatupa maisha yako. Unataka nini nakuuliza? Huna mali, huna nyumba, huna familia. Una maisha gani eti unayotaka kurekebisha?”
Simiyu aliachama kusikia kuwa nduguye amedinda kumsaidia. Hili ndilo aliloogopa zaidi. Na limetimika. Fundo la huzuni likamkaa moyoni kama nanga nzito. Akaamua kuondoka. Lakini akamuuliza Richard kuhusu shamba lake. Lazima baba alimgawia shamba hata kidogo kabla ya kifo chake. Richard alicheka na kusema kuwa baba hakumwaachia hata kikonde. Hana kwao.
“Tafuta maisha nje ya kijiji hiki. Huku si kwenu,” alimalizia Richard. Simiyu alilengwalengwa na machozi machoni. Hakuamini yaliyomfika. Richard ndiye mwanaye mkuu Mzee Shikhanda. Kulingana na mila na desturi, alikuwa mwenge wa maamuzi ya babake marehemu.
***** ***** ******
Simiyu hakuwa na budi kulala katika nyumba ya rafikiye Matendechero. Aliamua kuwa asubuhi angeanza safari moja kwa moja hadi Kakamega. Angefanya kazi za shokoa hadi apate fedha zitakazotosheleza ufunguzi wa karakana yake mwenyewe. Alijawa tumaini. Lazima hilo angetekeleza. Alijisemea akitabasamu.
Saa tano usiku, mlango ulibishwa. Polisi waliingia na kumkamata Simiyu. “Bwana David Simiyu, unakamatwa kwa madai ya kumwuua nduguyo Richard. Chochote utakachosema kitatumiwa dhidhi yako katika mahakama kwa hivyo una haki ya kusalia kimya…” Simiyu alichanganyikiwa. Matendechero alijaribu kuwasihi polisi wamwachilie kwani Simiyu alikuwa nyumbani kwake tangu saa kumi alasiri lakini hawakusikia. Simiyu alisindikizwa hadi kwenye karandinga ya polisi.
***** ****** *****
Wanakijiji waligutushwa na habari hii. Mbunge wao mpendwa kauawa na nduguye mwovu. Aah! Simiyu mwovu kweli… Simiyu kwa upande wake hakufua dafu kuwasihi polisi kuwa hakuhusika kwa vyovyote vile na kifo cha nduguye. Kulingana na ripoti ya mkewe wa pili Richard, Simiyu alisikika akimtishia maisha Richard kwa sababu alikataa kumpa pesa na shamba la kujistawisha. Simiyu hakuamini amepagaziwa shutuma za uongo.
Mahakamani, hakuwa na wakili. Matendechero ndiye alikuwa shahidi wake wa pekee. Naye alishindwa kumtetea vilivyo kutokana na maswali magumu ya kiongozi wa mashtaka. Hatimaye uamuzi ukatolewa. David Simiyu alifungwa miaka ishirini kwa madai ya kumwuua nduguye Richard. Jioni hiyo hiyo, alipelekwa hadi gereza la Kamiti mjini Nairobi. Akawaza tena. Maisha yake ni yepi? Au Richard alimwambia ukweli? Hana maisha. Anaishi kwa dunia hii kufanya lipi?
Majuma kadhaa baadaye, Matendechero alimwarifu kuwa alipata fununu ya kwamba mkewe wa pili Richard ndiye aliyetekeleza mauaji hayo na kumpoka mali marehemu mume wake. Yasemekana alitorokea nchini Australia miezi kadhaa baadaye…
Brian Nzomo ni mwandishi na mwanafunzi wa mawasiliano na uanahabari katika Chuo kikuu cha Kenyatta. Wasiliana naye kupitia anwani ya barua pepe: bryonzoms505@gmail.com