GRESI.

Na Brian Nzomo.

Wanafunzi wa darasa la sita walichoshwa na chuki niliyokuwa nayo dhidhi ya Gresi. Gresi alikuwa banati aliyesomea darasani kwetu ila alikuwa amepevuka kiumri kumpiku mwanafunzi yeyote yule. Alikuwa na umri wa miaka kumi na mitano, wengine wetu tulikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Alikuwa msichana mrefu ajabu mwenye umbo la janajike aliyefaa kuolewa katika kijiji chetu. Aghalabu, alikuwa mrembo si haba aliyewavutia vijulanga walioipa shule kisogo.

Kila mmoja pale darasani alimwogopa. Nami pia nilimwogopa sana na kumchukia. Sikupata kuzungumza naye hata mara moja, jambo lililowashangaza wenzangu. Kila waliponisaili kwa nini ningemwambaa kama tauni, ningewajibu kuwa

“Nahisi kuwa Gresi ana chembe za ushetani ndani yake, na roho wa mungu umenifunulia kuwa si vyema kutangamana naye…”

Wakati huo nilikuwa mkristo mwenye imani dhabiti na wenzangu walinihusudu sana kwa kuwa nilikuwa na ujuzi mwingi katika masuala ya bibilia. Hata hivyo walimaka sana,

“Ni imani ipi hiyo imfunzayo mtu kumchukia mwengine?”

Nilichukizwa sana na minong’ono ya wanafunzi wenzangu kila mwalimu alipodakiza kuwa ‘watu waliochukiana sana walikuwa wakipendana sana’. Walinitazama wakiangua vicheko kama wehu. Nilitanabahi kuwa walinidhania kumpenda Gresi. Fikra hizo zilinisibu kwa uchungu hadi pale nilipoamua kuwa nitamchukia Gresi wazi wazi.

Kwa kuwa nilikuwa kiranja pale darasani, nilianza tabia ya kumpa majukumu mazito Gresi. Nilizoea kumtia matatizoni na walimu. Jambo hilo lilinipa furaha moyoni, nilikuwa dhahiri kuwa hangedhubutu kunitenda lolote.

                          ***** ****** ****

“Kwa nini umenizoea sana?” Sauti nzito ya Gresi ilinijia pale darasani. Alikuwa amesimama mbele yangu mithili ya jitu. Alikuwa amekishika kiuno chake, uso wake ukidhihirisha kuwa alikuwa ameghadhabika.

“Nenda kaketi! Sina muda wa kupoteza kuzungumza na vimama wasiojiheshimu,” nilisema kwa madaha.

Uso wake ukabadilika. Tabasamu likamketi usoni. Kisha akaniambia,

“Wallahi! Leo utanitambua. Utajutia vitendo vyako dhidhi yangu. Nisipokusababishia kifo leo hii, basi nilaaniwe na ibilisi! Jioni hii tupatane pale nje ya shule, nitakucharaza kama mbwa koko, ngoko ya tumbiri wewe!”

Kwa kuwa nilikuwa kiranja pale darasani, nilianza tabia ya kumpa majukumu mazito Gresi. Nilizoea kumtia matatizoni na walimu. Jambo hilo lilinipa furaha moyoni, nilikuwa dhahiri kuwa hangedhubutu kunitenda lolote

Maneno yale yalinichoma kana kwamba moyo wangu ulikuwa makuti. Nilitaka kusimama na kumwarifu mwalimu, hata hivyo, machochezi ya wanafunzi wengine yalinipa hofu. Iwepo ningekataa kujihusisha na vita vile, ningeishi kuwa mwoga machoni pa wanafunzi wenzangu. Ila kupigana naye Gresi, ingekuwa vigumu kwangu kushinda.

Siku nzima nilihisi kutokuwa na amani. Wanafunzi wa darasa la sita hata hivyo waliisubiri kwa raghba vita vile. Walijua wazi kuwa ningepondwa kama kitoto kidogo lakini hawakujali wala kubali.

Nikajipa moyo. Mimi ni mvulana. Nina nguvu na siha zilizopiku za msichana huyu. Hawezi kunishinda. Lazima nitang’ang’ana.

Siku haiwi mrefu. Jioni ikafika hatimaye.

                *****      ******    *******

Uga wa vita ukaamuliwa. Kiwanja kimoja kilichojaa magugu si haba. Gresi akatua mkoba wake ardhini na kuvua sweta lake. Akaivua blauzi yake nyeupe. Akasalia na fulana nyekundu akajiweka tayari. Akaruka ruka upesi huku madodo yake mabivu yalikuwa yanatetemeka kwa mvuto.

Vikelele vikaanza huku wavulana wenzangu wakaanza kunipa motisha. Nikaikunja sura na kuiweka taswira ya hasira. Hata hivyo, moyo wangu ulisheheni hofu. Nikamtazama Gresi. Janajike kweli kweli. Nimesimangwa na wasichana wenzake.

Nilivua shati langu nikabaki kifua tupu. Nikavikumbata viganja vyangu na kuyaweka makonzi tayari. Kilichofuatia kilikuwa kimbunga.

Kabla nilirushe ndondi, kifua kizito kilinipiga dafrau. Nilibwagwa ardhini ajabu nikapoteza ufahamu kwa muda. Niliporejea ulimwenguni, Gresi alikuwa juu yangu. Masumbwi mazito yaliniwanga kichwani. Nikapiga mayowe. “Nisaidieni! Ananiua!”

Lakini wapi! Walisherehekea. Walifurahishwa ghaya na vitimbi hivyo. Nilishindwa kupata nafasi ya kumwondoa juu yangu. Mguso wake badala yake ukanipa hisia za ashiki. Mlingoti wangu ukasimama. Ikawa mchanganyiko wa hisia za hamu na maumivu.

“Mwalimu yaja! Kimbieni!” Mwanafunzi mmoja akapaza sauti na kuchomoka pale mara moja. Wanafunzi wengine walinafasika kuondoka pale. Tuliosalia tulikamatwa na kurejeshwa shuleni kupokea kichapo.

Chuki yangu ikawa maridhawa. Nilimwambaa kabisa Gresi hadi nilipomaliza shule yangu ya msingi. Nilifaulu kusomea shule ya sekondari iliyokuwa mbali na wilaya yetu. Hata nyakati za likizo, sikupata habari zake Gresi tena. Fununu zilisema kuwa alishindwa na masomo akaolewa naye dereva wa magari yasafirishayo miraa.

***** ***** *****

Kisa hicho nilikisahau kabisa. Kwa zaidi ya mwongo mmoja, vioja vya utotoni vilipotea kabisa akilini mwangu. Hadi pale nilipokutana naye Gresi.

Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka ishirini na minne. Nilikuwa nasomea shahada ya uzamili katika chuo kikuu. Nilirejea kijijini kufanya utafiti. Gresi alikwisha vunja ndoa yake. Alikuwa chifu wakati huo. Tulikumbana njiani akiwakaripia walevi wa chang’aa na kuwazaba makofi mazito.

Alinisalimu kwa heshima, tukazungumza kuhusu maisha baada ya shule ya msingi. Tulipoagana ndipo nilipokumbuka yaliyotendeka jioni ile. Nikajichekea tu…

Brian Nzomo ni mwanafunzi wa mawasiliano na uanahabari katika chuo kikuu cha Kenyatta. Wasiliana naye kupitia barua pepe: bryonzoms505@gmail.com

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started